Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Vasily Nebenzya, mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa alitangaza siku ya Alkhamisi kuwa, rasimu ya azimio la Marekani la kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran haina uwezekano wowote wa kupitishwa katika Baraza la Usalama. Kwa mujibu wa Nabenzya, hatima ya utekelezwaji wa azimio kama hilo ni kuvunjika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Amesema, ni wazi kwamba Iran haitalikubali azimio hilo na ina haki ya kulikataa. Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Russia amesisitiza kuwa, wakati Marekani ilipoanza kuandaa azimio hilo, nchi yake iliitanabahisha kuwa halina uwezekano wowote wa kuweza kupitishwa.
Tangu katikati ya mwaka uliopita wa 2019, Washington imeanzisha vita vikubwa vya kisaikolojia ili kuweza kupata matilaba yake, ambayo ni kuendeleza vikwazo vya silaha dhidi ya Iran; vita ambavyo vinaendelea hadi sasa. Viongozi waandamizi wa Marekani na hasa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Mike Pompeo, amekuwa akidai katika matamashi anayotoa mara kwa mara kwamba, kuhitimishwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran kutachochea mashindano ya silaha katika eneo la Asia Magharibi, kutaimarisha nguvu za Iran na waitifaki wake katika eneo na kuhatarisha usalama wa utawala wa Kizayuni.
Katika hatua iliyofuata serikali ya Trump ikakita na kuelekeza juhudi zake katika kuzishawishi nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zikubaliane na takwa lake, kwa kuwasilisha rasimu ya azimio mbele ya baraza hilo, linalotaka vikwazo vya silaha dhidi ya Iran virefushwe. Azimio lililopendekezwa na Marekani linataka Iran ipigwe marufuku kuuza na kusafirisha silaha au vifaa vinavyohusiana na silaha. Azimio hilo linazipiga marufuku pia nchi zingine kuiuzia na kuipatia Iran silaha au vifaa vinavyohusiana nazo, isipokuwa kama suala hilo litaafikiwa na kamati maalumu katika Baraza la Usalama. Si hayo tu, rasimu ya azimio lililopendekezwa na Marekani inasisitiza kuwa, endapo nchi zingine zitakuwa na sababu zenye uzito wa kuhisi kwamba shehena yoyote ya bidhaa inayosafirishwa kutoka nchi hizo ina uwezekano kuwa imebeba bidhaa ilizopigiwa marufuku Iran, ziifanyie upekuzi shehena hiyo. Kwa kutumia sababu kama hizo, azimio hilo vilevile linazitaka nchi zingine zisimamishe na kuzipekua meli zinazofanya safari katika maji ya bahari huru ya kimataifa. Rasimu ya azimio lililopendekezwa na Marekani inatilia mkazo pia kukamatwa na kuzuiwa mali zao na kupanga kuwawekea marufuku ya kusafiri watu wanaokiuka vikwazo hivyo vya silaha.
Kupitishwa azimio hilo kunahitaji kura tisa kati ya 15 za wanachama wote wa Baraza la Usalama pamoja na kutopigiwa kura ya veto na nchi wanachama wa kudumu, hususan Russia na China. Kuhusiana na hilo, msimamo ziliotangaza hadi sasa Moscow na Beijing unaonyesha kuwa nchi hizo mbili zitalipigia kura ya turufu azimio hilo lililopendekezwa na Marekani. Maafisa wa madola hayo mawili makubwa kimataifa ambayo ni washindani wa Marekani wameshasisitiza mara kadhaa kuwa wanalipinga azimio hilo na wazo la kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Maria Zakharova amesema, kurefusha vikwazo dhidi ya Iran si hatua chanya na ya kujenga. Ameashiria rasimu ya azimio lililopendekezwa na Marekani la kurefusha vikwazo hivyo na akasema: "Rasimu ya azimio hili ina vipengele ambavyo havina uhusiano wowote na hatua za kutatua masuala yanayohusu shughuli za nyuklia za Iran. Azimio hili linajumuisha uchukuaji hatua zinazoendana na sera ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran."
Licha ya muelekeo huo uliopo, maafisa wa serikali ya Trump wangali wanakazania kuendeleza mtazamo wao uliogonga ukuta wa kutaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran. Katika msimamo wa karibuni kabisa uliotangazwa na Marekani, Kelly Craft mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa, siku ya Alkhamisi alitangaza kuwa nchi yake itatumia kila wenzo kuhakikisha Baraza la Usalama linarefusha vikwazo vya silaha ilivyoekewa Iran. Craft amedai kuwa, ikiwa vikwazo hivyo havitarefushwa, Tehran itatuma silaha nyingi zaidi kwa waitifaki wake na makundi yake ya niaba katika eneo. Kwa anavyodai Craft, suala hilo linakwenda mbali zaidi ya kuwa kadhia inayohusu usalama wa nchi za Asia Magharibi kwa kuathiri pia usalama wa vikosi vya jeshi la Marekani katika eneo hilo. Matamshi hayo yanaonyesha kuwa, Marekani inatumia kila mbinu kuendesha propaganda chafu dhidi ya Iran ili kuchochea hisia za hofu kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu kwa kutaka iaminike kuwa, kuimarika zaidi nguvu za kiulinzi za Iran ni tishio na hatari kwa nchi za eneo hili; ilhali siasa na hatua za Marekani katika eneo hususan zilizochukuliwa katika kipindi hiki cha uongozi wa Trump zinaonyesha kuwa, Washington ndio chanzo hasa cha kuvurugika uthabiti na kukosekana amani katika Asia Magharibi.../
342/